MAKALA



Wanafunzi roho mkononi usafiri wa daladala Zanzibar.







Siku ya alhamis Novemba 26, 2012 konda wa daladala alinichoma kisu, kisa nilimlipa nauli sh 150 ambayo yeye haitaki, ” anasema Kassim Juma.
 
Kassim ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Hurumzi Zanzibar. Anaeleza jinsi wanafunzi wanavyofanyiwa vitendo vya udhalilishaji katika usafiri wa daladala.
 
Katika siku hiyo anasema , alikuwa anatoka shule kuelekea nyumbani kwao Fuoni. Alipanda usafiri wa daladala katika kituo kikuu cha daladala kiitwacho Darajani ndipo alipokumbana na mkasa huo.
 
Akiwa katika daladala hiyo ya Fuoni, anasema alipofika katika kituo kidogo cha daladala Michezani Kisonge, konda wa daladala hiyo, aliomba alipwe nauli na abiria waliokuwemo kwenye gari hiyo.
 
Baada ya kufika zamu yake ya kulipa, anasema kuwa alimpa sh.150 wanayopaswa kulipa wanafunzi, lakini konda huyo hakuitaka kabisa fedha hiyo na kumtaka alipe nauli ya abiria kamili sh. 300.
 
Alisema baada ya kumjibu kuwa hana sh. 300 ndipo  alianza kumtolea maneno ya kashfa na kuanza kumpiga.
 
“ Alipoanza kunipiga nami sikukubali nikampiga kisha tukaanza kupigana, lakini alinizidi nguvu na kuchukua kisu kisha akanichoma usoni juu ya pua,”alisimulia.
 
Wakati hayo yakifanyika, anasema kuwa basi hilo lilikuwa limesimama kituoni ili kupakia abiria wapya lakini baada ya kufanya kitendo hicho basi hilo lilikimbia.
 
Alichofanikiwa kukifanya ni kunakiri namba ya basi hilo kisha kwenda kuripoti katika  kituo cha polisi Mwanakwerekwe. Huko alipewa PF3 kwa ajili ya kwenda kutibiwa hospitali.
 
Polisi walilitafuta basi hilo na kufanikiwa kulipata kisha muhusika akafunguliwa kesi na kupelekwa mahakamani.
 
Tukio hilo anasema kuwa ,lilimuathiri sana kiafya kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata ambayo hadi sasa kipindi cha baridi anahisi maumivu makali.
 
Kilichomsikitisha zaidi anasema kuwa, kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani alihisi kuwa hatendewi haki kutokana na usumbufu aliokuwa anaupata.
 
Hii ni kutokana na ukweli kuwa, kila mara kesi hiyo inaposikilizwa ,hakimu alikuwa anataka ushahidi zaidi, licha ya mtuhumiwa kukiri mbele ya mahakama na kuwepo uthibitisho wa daktari aliyemtibu.
 
“Baada ya kuona kila siku nahangaishwa na kuupoteza muda mwingi mahakamani huku masomo  yananipita niliamua kuifuta kesi hiyo na kumsamehe mtuhumiwa,”alisema.
 
Kassim Juma anasema, tukio hilo ni mojawapo ya matukio kadhaa wanayofanyiwa wanafunzi wanaotumia usafiri wa daladala, ikiwemo kusukumwa , kupigwa vibao na kuvuliwa juba kwa wasichana.
 
Kwa muda mrefu, wanafunzi wa shule za smingi na sekondari Zanzibar  wanaotumia usafiri wa daladala wamekuwa wakilalamika kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji, lakini suala hilo bado halijapatiwa ufumbuzi.
 
Vitendo hivyo, vimekuwa vifanywa hadharani kwa sababu moja ama nyingine, ikiwemo wanafunzi hao kutolipa nauli kamili ya abiria sh.300.
 
Mwanafunzi mwingine Aisha Juma Ali wa shule ya sekondari Haile Selassie, anasema adha wanayoipata kwa kutumia mabasi ya umma ni kubwa, hivyo kuitaka serikali ichukue hatua za haraka kudhibiti mwendo huo.
 
 
“ Wanafunzi kwa kweli tunadhalilishwa na baadhi ya wenye daladala ambao wakiona wanafunzi huwa hawataki kusimama kutupakia wakati mwengine tunapojaribu kuingia kwa nguvu wanatupiga na kutusukuma,” alisema Aisha.
 
Aliiomba serikali kutilia mkazo, uamuzi wa wanafunzi kulipa nusu nauli ili waondokane na usumbufu wanaoupata.
 
Alisema baadhi ya makonda na madereva wamekuwa wanakataa kuwapakia na wanapowapakia daladala hugeuzwa kuwa kama darasa kutokana na wingi wa wanafunzi.
 
Naye mwanafunzi Muhammed Omar Said alisema wanaosumbuka zaidi na tatizo hilo, ni watoto wa maskini wanasoma shule za serikali.
 
“Nyumbani napewa sh 300 kwa ajili ya kutumia natoka nyumbani nikiwa sijala kitu, lakini unapofika katika daladala konda hataki kunipakia kwa sababu sina nauli ya sh.300,” alisema mwanafunzi huyo.
 
Aliiomba serikali kuwatafutia mabasi maalum za wanafunzi au kuzungumza na makonda na madereva wa mabasi ya abiria, kuacha kuwanyanyasa wanafunzi na kuwapakia katika daladala bila ya usumbufu wowote.
 
“ Unapojaribu kusimamisha daladala hawataki kusimama hasa wakituona tumevaa sare za shule,”alisema Omar.
 
Alibainisha kuwa husimama vituoni kwa muda mrefu na mara nyingi daladala husimama wanapoona abiria ambao sio wanafunzi na wao huitumia nafasi hiyo kupenya kwenye daladala.
 
Baada ya kuitumia nafasi hiyo, kinachofuata kwa makonda ni matusi, kuwasimanga hata wakati mwingine huthubutu kuwashusha.
 
Katibu wa serikali za wanafunzi Zanzibar (Usewaza) Salum Humoud, alisema kuwalipisha wanafunzi nauli kamili ni kukiuka  kanuni ya magari ya biashara kifungu cha 80 cha sheria namba saba ya usafiri barabarani ya mwaka 2003.
 
Kanuni hiyo alisema kuwa, inatambua kuwepo kwa  wanafunzi, wazee na watu wenye ulemavu kulipa nusu nauli.
 
Aliwataka wanafunzi watakaotozwa nauli kubwa, kuandika namba za gari kisha kutoa taarifa kituo cha polisi ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
 
Katibu wa Umoja wa Daladala Unguja, makame Ali Makame alisema kuwa, ni kweli kuna malalamiko mengi ya muda mrefu wanafunzi kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji katika daladala.
 
Alishangazwa na baadhi ya makonda na madereva wenye tabia na kuwataka wafuate agizo la serikali kuwa wanafunzi wote walipe nusu nauli.
 
Alisema endapo itathibitishwa kuwa gari la abiria limekiuka sheria litachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungiwa kufanya biashara.
 
Alisema wanafunzi ndio taifa la kesho hivyo wasiojua thamani ya elimu kwa watoto ni jambo la kusikitisha sana kwa kufanya vitendo vya unyanyasaji kwa wanafunzi.
 
Alisema, serikali imefika wakati kulishughulikia suala hilo ambalo ni la muda mrefu na wanafunzi wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa.
 
Ali Muhammed Juma ambaye ni dereva wa daladala ya njia ya Kiembe samaki alisema kuwa, baadhi ya madereva na makonda wamekuwa na udhaifu huo na hawana ubinadamu kwa kukataa kuwabeba wanafunzi au kuwatoza nauli ya abiria kamili.
 
“ Najitahidi sana kuwafahamisha madereva wezangu wasiwadhalilishe wanafunzi kwani hao ndio wataweza kuwasaidia katika maisha ya baadaye,”alisema.
 
Abubakari Khamis konda wa daladala njia ya daraja ya Bovu alisema kuwa, mwanafunzi ni abiria kama abiria wengine na wanapowabeba hupata hasara kwa kushindwa kumudu gharama za uendeshaji.
 
“ Gari yangu naruhusiwa kupakia abiria 20 kwa maana hiyo kila abiria nauli ni sh 300 natakiwa nipate sh.6000 kwa mzunguko mmoja sasa nikisema nipakie wanafunzi kwa sh.150 ni hasara ,”alisema Khamis.
 
Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi  wa jimbo la Bububu, Hussein Ibrahim Makungu, alisema baada ya kuona wanafunzi wanadhalilishwa kwenye usafiri wa daladala, aliamua kununua gari maalum kwa ajili ya wanafunzi katika jimbo lake.
 
“ Nimeshashudia mwanafunzi akisukumwa na kupigwa, kisa hajalipa nauli.Kitendo hicho sitoweza kukisahau katika maisha yangu. Kilinisikitisha sana ndipo nikaamua baada ya kupata ridhaa ya wananchi wa jimbo langu nikaamua kununua mabasi mawili kwa ajili ya wanafunzi katika jimbo langu,”alisema .
 
Magari hayo yanabeba wanafunzi kuwapeleka shule na kuwarejesha nyumbani kwao bila ya malipo yoyote.
 
Kila gari  alisema kuwa, linabeba wanafunzi 320 bila ubaguzi wowote huku kila mwezi analazimika kulipa sh. milioni mbili na laki mbili gharama za mafuta ya magari hayo.
 
Pia hulazimika kutoa fedha nyingine kwa ajili ya kuwalipa dereva na konda wanaohudumia magari hayo  kuwapeleka wanafunzi shule na kuwarejesha.
 
Mkurugenzi wa idara ya usafiri na leseni Suleiman Kirobo, alisema kuna makundi maalum yanayotakiwa kutozwa nusu nauli katika usafiri wa magari ya abiria.
 
Makundi hayo ni wanafunzi,watu wenye umri mkubwa na wenye ulemavu.
 
Aliitaka jamii inapoona watu hao wanafanyiwa vitendo vya unyanyasaji katika magari ya abiria kutofumbia macho vitendo hivyo.
 
“ Wakati mwingine katika gari za abiria, mwanafunzi anafanyiwa vitendo vya unyanyasaji, lakini abiria kwenye magari hayo wanakaa kimya bila ya kukemea au kuripoti vitendo hivyo sehemu husika,”alisema Kirobo.
 
Alifahamisha kuwa, endapo dereva au konda wa gari ya abiria ikithibitika kuwa, amewafanyia vitendo vya udhalilishaji kwa wanafunzi, watu wenye ulemavu na wazee watafungiwa wasiendelee kufanya biashara hiyo au kutozwa faini.

No comments:

Post a Comment