Simba yaiendea kambini Azam.

Wachezaji wa Simba wakiwa chini ya Kocha Mkuu, Mserbia Goran Kopunovic, wanatarajia kuingia kambini leo kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya Azam itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Manara, alisema baada ya kuwapa mapumziko ya siku mbili, wachezaji wa timu hiyo wataanza mazoezi leo jioni kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu Mlimani.
Manara alisema wanafahamu umuhimu wa mchezo huo na watajipanga kuhakikisha wanapata pointi zote tatu na kuendeleza heshima ya klabu yao msimu huu baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa ligi kama walivyotarajia wakati wanaanza msimu.
Alisema kila mechi iliyobakia kwenye ligi hiyo kwao ni sawa na fainali hivyo wanawakumbusha wachezaji wao umuhimu wa kufanya mazoezi kwa kiwango cha juu ili waweze kufanya mashambulizi kuanzia dakika ya kwanza hadi mwisho wa mchezo.
"Kikosi kilipumzika na kesho (leo) ndiyo tutaanza mikakati ya kuimaliza Azam, tunaijua na wao wanatujua, mechi zote zilizobaki ni sawa na fainali na kamwe haturudi nyuma kama tulivyozoeleka mwanzoni mwa msimu," alisema Manara.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 huku Simba ikianza kufunga na mabingwa hao watetezi walifanikiwa kusawazisha, hivyo kugawana pointi.
Simba itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 iliyoupata dhidi ya Ndanda FC kutoka Mtwara wakati Azam yenye iliwapa kichapo cha 4-0 Stand United ya mkoani Shinyanga.
Timu hizo mbili bado zinawania nafasi ya pili ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho wakati vinara Yanga leo wakiibuka na ushindi watatangazwa mabingwa wapya wa msimu huu.
No comments:
Post a Comment